Saturday, March 18, 2017

Namna ya kupata wateja

Katika ushindani wa kibiashara uliopo na mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia, kupata wateja kumekuwa kugumu sana. Hivyo ili ufanikiwe kweli katika biashara inabidi sio tuu uwe na bidhaa nzuri lakini pia ujue namna bora ya kutafuta wateja.

Hata kama una duka la nguo tuu dogo au saluni waweza kuwa umeathirika na namna ambavyo ushindani wa biashara ulivyo. Hivyo katika makala hii utajifunza mbinu ya kisasa kabisa ya kupata wateja wa biashara yako.

Kabla ya kujifunza  mbinu ya jinsi ya kupata wateja unahitaji kujua kwanza kwanini ni ngumu kupata wateja.

Hali ngumu ya kiuchumi : Kuna namna mbili ambapo hali ya kiuchumi inaweza athiri kupatikana kwa wateja. Kwanza kuwafanya wasiwe na uwezo wa kulipia bidhaa yako , na pili kuwafanya wajifikirie sana kuhusu kununua bidhaa zako. Katika yote haya hali ngumu ya kiuchumi inajenga ukinzani wa wewe kujenga ushawishi kwa wateja wako kununua bidhaazako.

Mabadiliko ya teknolojia: Teknolojia inafanya watu wengi zaidi waweze kuwafikia wateja wako ambapo hapo kabla haikua rahisi. Enzi hizo ilikua utengeneze vipeperushi au uwe na hela za kutosha kutangaza redio, kwa tv na kwenye mabango. Ila sasa watu kupitia Facebook, WhatsApp, na Instagram wanaweza kuwafikia watu wengi kwa urahisi. Hata yule mtengeneza keki mtaani kwenu nae yupo Instagram akitangaza keki na mikate yake. Bwana Mangi nae yupo kwa Facebook akitafuta wateja wa kibanda chake cha kuuza vocha za simu na MPESA.

Njia ya kisasa ya kisasa ya kuwapata wateja:

Tumefika wakati ambapo wateja wengi wana taarifa nyingi kuhusu wapi na kwa bei gani bidhaa zinapatikana. Hivyo wewe kuwa tuu na bidhaa fulani au kwa bei fulani hakutoshi kuwa njia ya kuwafikia.

Pia kwakua kuna watangazaji wengi wa bidhaa inakupasa wewe kuwa na namna ya kipekee ya kuwafikia wateja wako bila kuwa kero kwa wateja kama walivyo watu wengine wengi ambao ni wazi kabisa kwa “makelele” yao ya matangazo wanaonekana wazi wanachotaka wao ni kuuza tuu hizo bidhaa waishie zao. Ni ukweli wa kitaalamu katika marketing kuwa watu wengi  hawapendi kujisikia kuwa fulani anawauzia bidhaa. Hata hivyo hivyo haimaanishi kuwa watu hawapendi kununua. Watu hupenda kununua ila hawapendi ile hali ya kuwekwa “kati” na mtu anayejaribu kuwauzia kitu.

Ukichanganya na ukweli huo kuwa watu hawapendi kujisikia wakiuziwa bidhaa, halafu hali ngumu ya uchumi na mabadiliko ya teknolojia yanafanya kuwepo na “makelele” ya wafanyabiashara wengi,  basi wewe unahitaji mbinu ya ziada.

Hivyo basi mbinu ya kisasa ninayozungumzia hapa ni kutengeneza ushirika na wateja kama jamii ambayo itakuamini na kukuona una kitu zaidi ya kutaka tuu kuwauzia bidhaa zako. Kwa mbinu hii unajenga uhusiano na kufikia hisia za wateja wako, unatambua matatizo yao , unakua kweli mshirika wao katika yale ambayo unaona wao wanaweza kunufaika kupitia bidhaa zako hapo baadae.

Kwa mfano kama wewe ni muuza nguo, badala ya kila wakati kuwatangazia tuu mzigo mpya ulio nao, tambua kwanini hawa watu wanunue nguo mpya. Zungumza nao kuhusu hayo mambo. Mfano iwe ni swala la kujisitiri, au unadhani wananunua sana kwa ajili ya kujionyesha kuwa wanaenda na wakati na ni watu wa mitindo, basi waonyeshe unalielewa hilo kwa kutumia mitandao ya kijamii ukipost vitu vinavyoendana na hayo mambo ya mitindo na kuenda na wakati.

Jiweke katika nafasi zao, na uwahudumie vema kihisia kwanza , ukishawaonyesha kuwa wewe unaweza na unajua nini wanataka , hapo ni rahisi kuwaambia kuhusu bidhaa zako ambazo zitawafikisha katika malengo hayo wanayodhamiria.

Kwa mbinu hii unaondoa upinzani wa wateja kutaka kukusikiliza , na unafanya rahisi kwa wao kufanya maamuzi ya kununua bidhaa zako kwakua hawaoni kama unawauzia bidhaa, bali wanaona ni muendelezo wa ukaribu wako na utayari wako wa kuwaona wakijisikia vizuri na kufikia malengo yao.

Katika kutengeneza huo ukaribu wako na wao kupitia machapisho, videos, na picha mbalimbali wenyewe wateja wajisikia utayari wa kukutafuta. 

No comments:

Post a Comment